James 2

Onyo Kuhusu Upendeleo

1 aNdugu zangu, kama waaminio katika imani ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, Bwana wa utukufu, msiwe na upendeleo kwa watu. 2 bKwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, 3nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” 4 cje, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu?

5 dNdugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? 6 eLakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? 7Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa?

8 fKama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. 9 gLakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji. 10 hKwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote. 11 iKwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.

12 jHivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru. 13 kKwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.

Imani Na Matendo

14 lNdugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 mIkiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 nmmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 oVivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

18 pLakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”

Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo.
19 qUnaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.

20 rEwe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? 21 sJe, Ibrahimu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaka madhabahuni? 22 tUnaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. 23 uKwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Ibrahimu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. 24Mnaona ya kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.

25 vVivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.
Copyright information for SwhKC